BIMA YA AFYA NI MUHIMU KWA UHAKIKA WA MATIBABU - MAKALLA

Apongeza matumizi ya TEHAMA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuweka mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili wawe na uhakika wa matibabu wakati Serikali ikikamilisha mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amepongeza juhudi za NHIF katika kuimarisha huduma na utoaji taarifa kwa wanachama kwa njia ya kidijitali.

Hayo ameyasema leo katika Maonesho ya Kimataifa ya 46 ya Sabasaba katika viwanja vya Mwalimu Nyerere alipotembelea banda la NHIF na kuona huduma zinazotolewa na NHIF kwa wananchi.

"Kazi mnayofanya ni nzuri na kubwa na kwa sasa tuweke mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi wakati suala la Bima ya Afya kwa Wote likiendelea na mchakato, mimi ni mwanachama wa NHIF na kadi yangu inanipa uhakika wa matibabu, ni muhimu wananchi wakawa na bima ya afya" alisema Mhe. Makalla.

Akimkaribisha bandani hapo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Bi. Anjela Mziray alieleza kuwa Mfuko umejipanga kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa sasa wanaweza kupata taarifa mbalimbali za kihuduma na kujisajili kupitia mtandao.

"Tumefanya maboresho makubwa ambayo yanamuwezesha mwananchi kupata huduma ya kujiunga, kuangalia vituo anavyoweza kupata huduma na taarifa zingine kupitia NHIF App" alisema Bi. Mziray.

Alisema kwa sasa mwananchi ama mwanachama hana sababu ya kufika katika ofisi za Mfuko na badala yake anaweza akapata huduma alipo kupitia simu yake ya mkononi.

Mwisho.