Na Mwandishi Wetu, Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, ameweka wazi kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utafanikiwa kutokana na Imani kubwa iliyopo juu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Akiteta na Bodi ya NHIF, iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Bw. Eliud Sanga na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka, alisema “Nina Imani kubwa sana na uongozi wenu NHIF kwa kuwa mna uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa masuala yanayohusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii,” alisema.
Mhe. Mtaka aliongeza kuwa uwepo wa viongozi hao umeleta mabadiliko makubwa sana hivyo kuna mwanga mkubwa wa kufanikisha ndoto ya wananchi kuwa katika mfumo wa bima ya afya.
Aidha, Mhe. Mtaka alitoa wito kwa Bodi ya NHIF kutumia nafasi yao katika kumshauri Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya nchini juu ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Katika hatua nyingine aliutaka Mfuko kuangalia uwezekano wa kuanza kutoa elimu ya afya kwa vijana wa kizazi cha sasa ambao wengi hawajali afya zao kwa aina ya maisha wanayoyaishi ikiwemo ulevi, madawa ya kulevya ili kusaidia kupunguza gharama za matibabu mara wanapopata magonjwa makubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka aliyepo kulia akijadili jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Bw. Eliud Sanga.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi mjumbe wa Bodi Dkt. Zubeda Chande alipongeza ushirikiano wa ofisi ya NHIF Njombe na Serikali na kuahidi kwamba ushauri uliotolewa na Mkuu wa mkoa umepokelewa na Mfuko upo tayari kwa ajili ya utekelezaji.
"Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa".