NHIF, Mawakala wa Bima wazindua mpango wa ushirikiano kusajili wanachama

Imewekwa: 13 August, 2025
NHIF, Mawakala wa Bima wazindua mpango wa ushirikiano kusajili wanachama

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa pamoja na Chama cha Mawakala wa bima nchini (IAAT) leo tarehe 13 Agosti, 2025 wamezindua mpango wa ushirikiano kwenye eneo la usajili wa wanachama, ikiwa ni mkakati mahsusi katika utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote. 

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene C. Isaka amesema utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote umeanza rasmi mwezi Agosti, 2024 baada ya kupitishwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote pamoja na kanuni zake na kutangazwa katika gazeti la serikali.

Dkt. Irene amesema utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote, umeanza na wananchi mmoja mmoja au kipitia makundi mbalimbali wanaweza kujiunga na kunufaika na huduma za afya kupitia NHIF.

Dkt. Isaka aliendelea kusema,  Mfuko umewekeza katika Mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha taratibu za usajili wa wanachama na huduma za Mfuko bila ya kikwazo cha kufika katika ofisi za Bima ya afya.

Dkt.Irene alisema asilimia 87 ya watanzania wote wapo katika sekta isiyo rasmi huku asilimia 13 tu, ndio wapo katika sekta rasmi, ni wakati sasa wa kuwafikia katika maeneo yao kuwasajili na huduma za bima ya afya na kuwahakikishia uhakika wa matibabu wakati wote.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeingia makubaliano na Mawakala wa Usajili wa Bima nchini ili kuunza kusajili wanachama wa Bima ya Afya.
Pia amewakumbusha Mawakala hao kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kulinda taarifa za wanachama. Lakini pia aliwaadi ushirikiano katika kila hatua ikiwemo kila Meneja wa Mkoa kufanya mafunzo ya huduma za Mfuko ili Mawakala hao waweze kwenda kutoa elimu hiyo kwa wananchi kabla ya kuwasajili na huduma za NHIF. 

Hata hivyo Dkt. Isaka aliwajulisha Mawakala hao kuwa wanatakiwa kuwafikia wananchi na sio wananchi kuwafuata katika ofisi zao, vilevile mtizamo uwe kwenda kuuza vifurushi na sio kuuza magonjwa.
“tunakwenda kuuza vifurushi na sio magonjwa mwanachama aelezwe kwa undani kuhusu kifurushi na huduma ili kuweza kujiunga kwa wingi na kadiri tutakavyosajili wananchi wengi ndio watakasaidia wale wachache wanaougua kupata matibabu ya uhakika bila kikwazo cha fefha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Mawakala wa bima nchini (IAAT) Bw. Lugano Mkisi ameipongeza NHIF kwa kuchukua uamuzi wa kufanya kazi na Mamakala wa bima na kuahidi ushirikiano ili kuleta tija kwa wananchi.

Aidha alisema NHIF ina wigo mpana wa huduma na mtandao wa ofisi katika mikoa yote Tanzania bara ambao utatoa fursa kwa mawakala kuweza kutumia ofisi hizo za mikoa bila ya kutegemea kila kitu kufanyika makao makuu. 

Bw. Lugano alisema “sisi Mawakala wa bima tuna mtandai wa ofisi mpaka ngazi za jamii, hivyo kuwezesha  kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi, na pia kutumia ofisi za mikoa katika kutatua changamoto mbalimbali bila ya kutegemea makao makuu”.

Aliendelea kusema kuwa atasimamia mawakala kutoa huduma kwa weledi ili kuhakikisha Mfuko unaongeza idadi ya wanachama na kuwa Mfuko ya Bima ya Afya nchini inayotoa huduma bora kwa wanachama. 
Hata hivyo aliomba Mfuko kuendelea  kutoa mafunzo ya huduma zikizopo kwa Mawakala ili kuongeza uelewa wa Vifurushi vya NHIF na huduma ambazo mwanachama atanufaika nazo.

Alihitimisha kwa kusema kwamba katika robo hii ya kwanza ya mwaka wana mkakati wa kusajili Mawakala 300 kwa ajili ya mpanho uliozindu wa uandikishaji wanachama kwa niaba ya Mfuko ili kuweza kufikia lengo la kuongeza wigo wa huduma za bima ya afya kwa wananchi.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa