Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) limekutana na kufanya kikao kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kurahisisha utendaji kazi na kutoa huduma bora zaidi za bima ya afya kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika Aprili 25, 2025 katika Ukumbi wa Ngorongoro uliopo Arusha Mjini kwa kuwashirikisha wajumbe na wawakilishi kutoka Menejimenti ya Mfuko, Ofisi za Mikoa, TUGHE Taifa, Mkoa na Tawi la NHIF.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Bw. Eliud B. Sanga, amepongeza Menejimenti ya Mfuko kwa kuwa na chombo hicho maalum kinachotoa fursa kwa kila mtumishi kujadili masuala mbalimbali ya huduma za Mfuko.
“Nipongeze Menejiment kwa kuwa na chombo hiki muhimu cha kusimamia utawala bora kwa kuwa ni sehemu maalum ambapo mfanyakazi anapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na viongozi.” amesema Mwenyekiti wa Bodi.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi amesema kuwa Mfuko unahitaji watumishi ambao wanawajibika ili kuendelea kuwa na tija kwa Taifa. Alisisitiza kuwa Watanzania wengi sana wananufaika na huduma za NHIF, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunapunguza malalamiko ya wadau wa Mfuko wakati huo huo tukiendelea kupambana na vitendo vya udanganyifu dhidi ya Mfuko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka amesisitiza watumishi kudumisha amani kwa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao na pia kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2025.
“Nitoe rai kwenu watumishi kudumisha amani katika kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu 2025 na niombe kila mtumishi wa Mfuko kushiriki uchaguzi huo kikamilifu.”Alisema Dkt. Isaka.
Pia Dkt. Isaka alimhakikishia Mwenyekiti wa Bodi utayari wa watumishi wa Mfuko kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kuwezeshwa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupatiwa mafunzo, vitendea kazi na stahiki mbalimbali kwa wakati.