BODI YA NHIF YAFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI LINDI

Imewekwa: 25 June, 2025
BODI YA NHIF YAFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI LINDI

Leo, 23 Juni 2025 –Ujumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Eliudi Sanga  umefanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya NHIF Mkoa wa Lindi ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano kati ya Mfuko na Uongozi wa Mkoa, katika ziara hiyo ujumbe huo pia umefanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya NHIF mkoa wa Lindi.

Akizungumza na watumishi wa Mfuko Mwenyekiti wa Bodi Bw. Eliud Sanga alisisitiza kuhusu umuhimu wa uwajibikaji, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wateja ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika huduma za bima ya afya.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Zubeda Chande alilisitiza uadilifu kwa watumishi wa Mfuko katika njia Wanazotumia  kusajili wanachama ili kuepuka udanganyifu.

Dkt.Chande alilisitiza kwamba  "upatikanaji wa wanachama ni msingi muhimu wa uendelevu na uhai wa Mfuko hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha kuwa kila hatua inazingatia weledi na maadili ya kazi".

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF akisalimiana na watumishi wa Mfuko huo Ofisi ya Lindi akiwa katika ziara ya Bodi ya Wakurugenzi inayofanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka aliwakumbusha watumishi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria zilizowekwa kwani Mfuko hautosita kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kushiriki katika vitendo vya udanganyifu.

Dkt.Isaka aliendelea kusema kuwa  ziara hii inalenga kusukuma mbele ajenda ya mabadiliko ya kimifumo na uboreshaji wa huduma kwa wanachama wa NHIF.

Vilevile alitumia fursa hivyo kuwaonya  watumishi kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu dhidi ya Mfuko.
 
Ziara hii imeongeza chachu na ari kwa watumishi wa NHIF Ofisi ya Lindi huku uongozi wa Mfuko ukiahidi kuendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu, teknolojia na usimamizi ili kuhakikisha huduma za bima ya afya zinamfikia kila Mtanzania kwa ubora wa juu.

LINDI KUCHELE

"Bima ya Afya kwa Wote, jiunge sasa".