MADAI NHIF KUCHAKATWA KIDIJITALI

MADAI NHIF KUCHAKATWA KIDIJITALI Nov 08, 2024

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeanza kuchakata madai yanayowasilishwa na Watoa Huduma kidijitali ili kurahisisha ulipaji wa madai hayo, kubaini na kudhibiti mianya ya udanganyifu.

Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji ya Mfuko leo, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka amesema kuwa jumla ya Vituo 7,000 kati ya Vituo 10,004 vya Kutolea huduma za matibabu vilivyosajiwa madai yake yatachakatwa kwa Mfumo.

“Maboresho makubwa yanayofanywa kwenye Mifumo yetu yanakwenda kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo ya ucheleweshaji wa malipo ya Watoa Huduma kwa kuwa madai hayo yatachakatwa na Mfumo lakini pia tutaweza kubaini viashiria vya udanganyifu na kudhibiti kwa wakati,” alisema Dkt. Isaka.

Akitoa maelezo ya awali, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel aliihakikishia Kamati hiyo kuwa, Mfuko unafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha unashughulikia changamoto zilizokuwepo kwa kutrekeleza maagizo yanayotolewa na Mamlaka mbalimbali ili kufanikisha utoaji wa huduma bora, kuwafikia wananchi na kulinda uhai na uendelevu wa Mfuko.

Kwa upande wa Kamati hiyo iliyoongozwa na Mhe. Cecil Mwambe iliagiza kuanza utekelezaji wa suala la Bima ya Afya kwa wote ili wananchi waweze kujiunga na kuwa na uhakika wa matibabu wakati wowote.