Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wananchi wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuendelea kuboresha huduma zake na kuhakikisha wanachama wanapata huduma za bima ya afya kwa urahisi, ufanisi na kwa kutumia mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma.
Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 28, 2026 na wananchi waliotembelea banda la NHIF wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Homa ya Ini yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma, ambapo walipata fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko pamoja na kupata elimu ya bima ya afya.
Akizungumza katika maonesho hayo, Bw. Suleiman Rashid, mkazi wa Maili Mbili jijini Dodoma, alisema NHIF imepiga hatua kubwa katika kuboresha mifumo ya usajili, utambuzi wa wanachama na utoaji wa huduma, hali inayorahisisha wananchi kupata huduma za matibabu kwa wakati.
“Tunapongeza kwa kazi nzuri. Hakika NHIF ya sasa imepiga hatua kubwa katika maeneo mengi, likiwemo uboreshaji wa huduma zake, mifumo ya usajili na utambuzi, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wanachama wake," alisema Bw. Rashid.
Mbali na kuipongeza NHIF, wananchi wameitaka NHIF kuendelea kusogeza huduma karibu na jamii kwa kushiriki maonesho, mikusanyiko ya wananchi, makongamano na shughuli mbalimbali za kijamii ili kutoa elimu ya bima ya afya, kutatua changamoto zinazowakabili wanachama na kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na huduma za bima ya afya.
Katika banda la NHIF, wananchi pia walipata mafunzo kuhusu Mfumo wa Kujihudumia (Self Service), unaomwezesha mwananchi au mwanachama kujisajili, kufuatilia taarifa zake na kupata huduma mbalimbali kwa njia ya kidijitali bila kulazimika kufika ofisini.
Ushiriki wa NHIF katika maadhimisho hayo ni sehemu ya mkakati wa Mfuko wa kuendelea kuwafikia wananchi popote walipo kupitia maonesho, makongamano, ibada na mikusanyiko mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma hiyo.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa