NHIF YAIMARIKA, YATOA FARAJA NA MATUMAINI KWA WAZEE TANZANIA

Imewekwa: 01 October, 2025
NHIF YAIMARIKA, YATOA FARAJA NA MATUMAINI KWA  WAZEE TANZANIA

01 Oktoba 2025

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeshiriki maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani katika maadhimisho yaliyofanyika katika Viwanja vya Hekima vilivyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo ambayo yameratibiwa na shirika lisilo ya kiserikali la Philemon Foundation, yamewakutanisha wazee mbalimbali kwa lengo la kutambua mchango wao kwa ujenzi wa taifa.

Akizungumza wakati ya ufunguzi wa maadhimisho hayo Bw. Rodgers Mbaga ambaye ndio mratibu wa tukio hilo alisema, jamii inatambua mchango mkubwa uliotolewa na wazee hao katika kulifikisha taifa hapa tulipo, hivyo Philemon Foundation wameratibu maadhimisho hayo ili kuenzi mchango wa wazee hao. Aidha Bw. Mbaga alieleza umuhimu wa wazee kuendelea kutumiwa katika nyanja mbalimbali ili uzoefu wao uendelee kulinufaisha taifa. Pia aliwaekeza wazee hao umuhimu wa kujali afya zao ili waendelee kufurahia maisha yao, kwa kuzingatia hilo Philemon Foundation wamefanikisha ushiriki wa NHIF kwenye maadhimisho hayo ili wazee wapate fursa ya kupata elimu toka NHIF.

Kwa upande wa NHIF, Dkt. Paphael Mallaba aliyezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Dkt. Irene C. Isaka alisema NHIF ipo mstari wa mbele kutoa huduma za afya kwa wazee na ndio Mfuko pekee wenye wazee wanaonufaika na huduma za matibabu maisha yao yote baada ya kustaafu. Kwa kipindi cha miaka mitano 2020/21 hadi 2024/25 Mfuko umetumia jumla ya TZS. 407.38 bilioni kulipia huduma za afya kwa  wastaafu.

Aidha amesema NHIF ina fursa ya vifurushi mbalimbali ambapo wazee na watanzania wote wanaweza kujiunga na kupata huduma za matibabu bili kikwazo chochote. Dkt. Mallaba alikumbusha kuhusu gharama kubwa za matibabu pindi inapokosekana bima ta afya, hivyo aliwasihi wazee wasio na bima ya afya kujiunga na NHIF ili kuwa na uhakika wa matibabu hasa kipindi hiki ambapo serikali ipo katika hatua za utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Kwa upande wa wawakilishi wa wazee, wamepongeza namna NHIF inavyoendelea kuwajali wao na wenza  wao kupata huduma za matibabu hata baada ya kustaafu, wazee ambao bado hawana bima ya afya wameonesha nia ya kujipanga ili wajiungej kwenye vifurushi vilivyopo ili kunufaika na fursa hiyo.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa