Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda amepongeza maboresho mbalimbali yaliyofanya na NHIF katika utoaji wa huduma kwa Wanachama.
Alifurahishwa na uwepo wa mfumo wa NHIF Jihudumie ( NHIF Self-Service) mfumo unawawezesha wanachama na wadau wengine kujihudumia wenyewe mahali popote bila kufika ofisi za NHIF. Alisema hiyo ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Bi. Mwenda aliyasema hayo akipotembelea banda la NHIF kwenye maonesho ya wiki ya vijana jijini Mbeya. Aidha Bi. Mwenda aliahidi kuendekeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Taasisi hizi mbili.
Bi. Mwenda alisisitiza umuhimu wa NHIF na OSHA kuendelea kufanya kazi pamoja hasa kwenye eneo la mafunzo yenye lengo la kulinda usalama na afya za wafanyakazi, "Jitihada hizo zitapunguza kwa kiasi kikubwa wafanyakazi wanaopata changamoto za kiafya mahala pa kazi jambo litakalopunguza wagonjwa wanaohudumiwa na NHIF", alisema Bi. Mwenda.
Kwa upande wake Bw. Nicholaus Mwangomo, Msimamizi wa Ofisi ya NHIF Mkoa wa Mbeya alimshukuru Mtendaji Mkuu huyo kwa kutembelea banda la NHIF na kupata kufahamu huduma mbalimbali za NHIF na kufurahia huduma bora za bima ya afya.
Bw. Mwangomo alisema NHIF inatambua kazi inayofanywa na OSHA katika kusimamia usalama na afya mahala pa kazi, ambapo NHIF imekuwa ikinufaika na mafunzo mbalimbali toka OSHA.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa