Dodoma 12/11/2025
Menejimenti za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imepokea ujumbe wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi - Personal Data Protection Commission (PDPC). Ujumbe huo uliongozwa na Dkt.Emmanuel Mkiria Mtendaji Mkuu wa Kamisheni hiyo leo Jijini Dodoma
Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujenga mahusiano ya kimkakati yenye kulinda taarifa binafsi za Wanachama wa Mfuko hasa tunapoendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Akiitambulisha Taasisi yake katika kikao hicho, Dkt. Mkiria alisema, Taasisi hiyo imeundwa kwa mujibu wa Sheria na ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2022.
Dkt. Mkiria alisema NHIF ni miongoni mwa wadau wa kimkakati. Alielezea umuhimu wa majukumu ya PDPC hasa katika kipindi hiki ambapo teknolojia ya habari na mawasiliano imekua kwa kiwango kikubwa, hivyo kupelekea NHIF kuwa na hitaji la Kisheria la ulinzi wa taarifa binafsi za wanachama, jambo linalotiliwa mkazo hata kwenye Katiba ya nchi (haki ya faragha).
Kwa upande wa NHIF, PDPC imepanga kuweka mazingira wezeshi ili kuwezesha Mfuko na wadau wa NHIF kutunza taarifa binafsi Hivyo kikao kiliunda Kamati inayojumuisha Taasisi zote mbili ili kufanyia kazi maeneo ya kimkakati hususani: kujengea uwezo: Elimu kwa Umma: Concent Management System pamoja na Data Protection Impact Assessment.
Dkt. Emmanuel aliushukuru Uongozi wa NHIF kwa kutenga muda kukutana na PDPC kwa ajili ya kikao hicho muhimu.
Kwa upande NHIF Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene C. Isaka alimshukuru Mtendaji Mkuu wa PDPC kwa kufika NHIF yeye na ujumbe alioongozana nao.
Dkt. Isaka alitumia nafasi hiyo kuelezea namna NHIF ilivyojidhatiti katika kutunza taarifa binafsi za wanachama wake. Alisema, mpaka sasa watumishi wote wa Mfuko wamefanyiwa upekuzi (vetting) na mamlaka husika na wamekula viapo vya kutunza siri. Kwa upande wa Madaktari wa Mfuko pamoja na kufanyiwa upekuzi, pia wana viapo vya kutunza taarifa za wanachama kwa mujibu wa mabaraza ya taaluma yao.
Aidha Dkt. Isaka alisema NHIF inatambua umuhimu wa kulinda taarifa za wanachama, kwakuwa taarifa hizo ni bidhaa inayotafutwa sana ndani na nje ya nchi. Hata hivyo ujio wa PDPC ni fursa muhimu sana kwa Mfuko katika kujengewa uwezo zaidi wa kulinda taarifa binafsi za wanachama, ikizingatiwa adhabu kali zilizoainishwa kwenye Sheria ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pale inapotokea ukiukwaji wa Sheria hiyo.
Katika kikao hicho, pande zote zilikubaliana kuanza ushirikiano katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo (capacity building) watumishi wa Mfuko, ushirikiano kwenye utoaji wa elimu kwa umma hasa wadau ambao NHIF inafanya nao kazi kwa karibu.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa