Na Mwandishi Wetu – Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Akizungumza Agosti 12, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi katika Kumbi za Bunge mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, alisema utekelezaji huo umeanza na makundi maalum na unaenda sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Samizi, aliyewasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alisema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu muhimu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha afya ya wananchi na kujenga jamii yenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
“Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaenda sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii kwa kujenga jamii yenye afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,” alisema.
Alisema kuwa hadi kufikia Juni 2026, jumla ya kaya 276,004, sawa na asilimia 100 ya kaya zilizolengwa katika awamu ya kwanza, zilikuwa zimesajiliwa katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kati ya kaya hizo, kaya 185,973 zilikuwa tayari zimechukua kadi za uanachama, huku kaya 90,031 zikiwa bado hazijachukua kadi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya wanufaika kufariki na wengine kuhama maeneo yao.
Aidha, jumla ya wanufaika 997,015 walikuwa wamesajiliwa kati ya wanufaika 1,206,319 waliolengwa, sawa na asilimia 83 ya lengo.
Kati ya wanufaika hao, 495,034 walikuwa wamechukua kadi za uanachama, huku wanufaika 501,981 wakiwa bado hawajachukua kadi zao.
Serikali pia inaendelea na uhakiki wa wanufaika 209,304 kwa lengo la kuhakikisha taarifa zao zinakidhi vigezo vilivyowekwa na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote pamoja na miongozo ya utekelezaji.
Aidha alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwafikia wanufaika ambao tayari wamesajiliwa lakini hawajachukua kadi zao.
Alisema juhudi hizo zinafanyika kupitia Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri katika ngazi za mikoa, huku mbinu mpya ikihusisha matumizi ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii ili kurahisisha kuwafikia wananchi katika maeneo yao.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwafikia wanufaika 501,981 ambao tayari wamesajiliwa lakini hawajachukua kadi zao, kupitia Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri katika ngazi za Mikoa huku mbinu ya sasa ikiwa ni kutumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii,” alisema.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa wananchi waliokwishaingizwa kwenye mfumo wanapata fursa ya kutumia huduma za afya wanapohitaji, sambamba na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika upatikanaji wa kadi za uanachama.
Akizungumzia umarishaji wa Mifumo ya TEHAMA, alisema Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kupitia uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA na uunganishaji wa mifumo ya taarifa.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi katika usajili, uhakiki wa wanufaika na utoaji wa huduma, huku ikiendelea kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusiana na uanachama wa Bima ya Afya kwa Wote.
Akihitimisha taarifa yake, Mhe. Dkt. Samizi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa awamu ya kwanza wa Bima ya Afya kwa Wote.
Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuanza kutumika kwa Mfuko wa Usawa, elimu kwa umma kuhusu Bima ya Afya kwa Wote pamoja na kuboreshwa kwa mifumo ya TEHAMA kupitia uunganishaji wa mifumo ya taarifa.
Naibu Waziri huyo aliambatana na Menejimenti ya Wizara ya Afya, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe, na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka.
_1786552831.jpeg)
_1786552866.jpeg)