Bima ya Afya kwa Wote kuanza na kaya zisizo na uwezo

Imewekwa: 23 January, 2026
Bima ya Afya kwa Wote kuanza na kaya zisizo na uwezo

Waziri asisitiza uwajibikaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) ametangaza rasmi kuanza kutumika kwa Kitita cha Huduma Muhimu cha Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ya kwanza.

Amesema kuwa kitita hicho kitaanza kutumika Januari 26, 2026 kwa kundi litakalogharamiwa na Serikali. Haya ameyasema leo wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya kuhusu utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema kuwa suala la afya ni suala muhumi ambalo limebeba utu wa Mtanzania na mhimili wa maendeleo hivyo kila kiongozi ni lazima alibebe na kulifanya ajenda ya kudumu katika vikao vyote ili liweze kutekelezeka na kuleta matokeo chanya kwa afya za watanzania.
 

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa kulingana na maamuzi ya Serikali ya kuanza utekelezaji wa mpango huu kwa awamu, ni wajibu wa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kufanikisha maono haya ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

”Bila afya njema kwa wananchi ni ngumu kufanya mabadiliko yoyote ya kitaifa kwa wananchi wanaotumia muda mwingi hospitalini kuliko kazini. Hata teknolojia iwe ya kisasa kiasi gani, hata sera ziwe nzuri kiasi gani, bila watu wenye afya-hakuna mabadiliko yatakayodumu hivyo ni lazima hili tulitekeleze kwa nguvu zetu zote ili wananchi waweze kuwa na uhakika wa matibabu,” alisema Mhe. Mchengerwa.

Kutokana na hayo, amesema kuwa kutakuwa na uzinduzi wa kihistoria wa Bima ya Afya kwa Wote kabla ya kukamilika kwa siku 100 za Mheshimiwa Rais, uzinduzi ambao utabadilisha dhana ya haki ya huduma za afya nchini Tanzania na kuweka msingi mpya wa ulinzi wa afya ya Mtanzania. 

Aliwasisitiza viongozi hao kuwa kwa sasa ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote lazima iondoke kwenye ngazi ya waraka na iingie kwenye maamuzi ya kila siku ya uongozi wa Mkoa. 

“Lazima iwe ajenda ya kudumu katika vikao vya maendeleo, vikao vya usalama na vikao vya tathmini ya utendaji. Bima ya Afya kwa Wote isizungumzwe kama taarifa ya ziada; ijadiliwe kama ajenda ya msingi ya ustawi wa wananchi na uthabiti wa kijamii wa Mkoa,” alisisitiza Mhe. Waziri.

Aidha alitumia mwanya huo kusisitiza usimamizi wa zoezi la usajili wa wananchi katika ngazi zote hususan ya Kata, Kijiji na Mtaa. Alisema kuwa Mwananchi hapaswi kubaki nje ya mfumo kwa sababu ya uzembe wa mifumo, urasimu usio na sababu, au kutokujali kwa watendaji. 

Kutokana na haya alisema, uongozi wa kweli katika Bima ya Afya kwa Wote hautapimwa kwa idadi ya maagizo yaliyotolewa, bali kwa idadi ya wananchi walioguswa na mfumo, waliolindwa dhidi ya gharama za matibabu, na waliopata huduma kwa heshima. 

Alisema kuwa utekelezaji huu utafanikishwa kwa kuwepo kwa mfumo unasomana taarifa kwa vituo vyote vya kutolea huduma ili kupunguza gharama za uendeshaji lakini kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.

Akizungumzia gharama za kitita hicho, alisema itakuwa ni shilingi     150,000 kwa Kaya ya watu wasiozidi sita (6)     itakayojumuisha mwanachama mchangiaji, mwenza     wa mwanachama na wategemezi wanne (4).

“Wategemezi hao wanaweza kuwa ni mzazi wa mwanachama au mzazi wa mwenza wa     mwanachama; mtoto wa mwanachama wa kuzaa,     kuasili au wa kambo aliye na umri chini ya miaka     ishirini na moja; au ndugu wa damu wa     mwanachama aliye na umri wa chini ya miaka     ishirini na moja,” alisema.

Huduma za Kitita cha Huduma Muhimu kitatolewa kwa kuzingatia utaratibu wa Rufaa katika Vituo vya kutolea huduma za Afya vitakavyoingia Mkataba     na Skimu za Bima ya Afya.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa