Dar es Salaam,
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) leo wamesaini Mkataba wa utoaji wa huduma kwa wanachama wa ZHSF, ukiwalenga zaidi wanachama kutoka sekta isiyo rasmi waliopo Tanzania bara.
Makubaliano haya mapya ni mwendelezo wa ushirikiano ulioanzishwa mwezi Juni 2024, ambapo awali huduma zilikuwa zikitolewa kwa wanachama kutoka sekta rasmi pekee.
Hafla ya utiaji saini imefanyika jijini Dar es Salaam, ikihusisha Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dr. Irene Charles Isaka na Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF Bw. Yaasin Ameir Juma.
Viongozi hao wamekubaliana kubadilishana taarifa za wanachama ili kuwezesha wanachama kupata huduma bora na kwa urahisi. Vile vile wamekubaliana kuimarisha mifumo pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI) ili kukabiliana na udanganyifu.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wengi zaidi, hususan wale walioko nje ya mfumo rasmi wa ajira.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa