Nini siri ya bei za dawa zinazopangwa na NHIF?
Bei za dawa zinazotumika na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya zinapangwa kwa kushirikiana na watoa huduma na zinafanyiwa mapitio mara kwa mara. Hata hivyo, kutokana na kubadilika mara kwa mara kwa thamani ya fedha ya Tanzania inawezekana kabisa kuwa bei za dawa na vitendanishi ikabadilika kabla ya kikao cha mapitio hivyo kufanya bei zilizopitiwa awali kuonekana kuwa zimepitwa na wakati. Hata hivyo, juhudi zinafanyika ili kuiomba Serikali kuunda chombo cha kudhibiti bei za huduma za afya ili kupunguza uwezekano wa watoa huduma kupandisha bei kadri wanavyotaka.

Kwa nini vitambulisho vinachelewa kutolewa?
Utaratibu wa kupata vitambulisho vya Bima ya Afya unaanza kwa mwanachama kujaza fomu ya kuomba kitambulisho. Fomu hiyo ikishajazwa kikamilifu inatakiwa kuwasilishwa kwenye ofisi zetu za Mfuko zilizo karibu na mwajiri husika. Katika utaratibu wa kawaida kitambulisho cha mwanachama kinakuwa tayari ndani ya siku 21 za kazi tangu kuwasilisha fomu hiyo.

Hata hivyo, wakati mwingine fomu hizo zinachelewa kuwasilishwa katika ofisi zetu hivyo kusababisha pia wanachama kuchelewa kupewa Vitambulisho vyao. Hivyo tunawaomba wanachama na waajiri kutupa ushirikiano kwa kujaza fomu mara baada ya kuajiriwa na kuwasilisha fomu kwetu ili tuanze utaratibu wa kutengeneza vitambulisho.

Je unaweza kutueleza kwa ufupi nini maana ya Mifuko ya Afya ya Jamii na uhusiano wake naa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya?
CHF ni Mfuko wa Afya ya Jamii, ulioanzishwa kisheria kupitia Sheria Na 1 ya mwaka 2001 (SURA 409 ya Sheria za Tanzania) ili kutoa huduma za matibabu kwa jamii iliyopo katika sekta isiyo rasmi mijini na hasa vijijini katika ngazi ya halmashauri, tarafa kata na kijiji.

Ni utaratibu wa hiari unaoiwezesha kaya kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima kwa kuchangia mara tu kiasi cha shilingi 5,000.00 au 10,000.00 kwa kadiri jamii yenyewe katika Halmashauri husika itakavyoamua.

Serikali kwa upande wake inachangia kwa kiwango ambacho kaya inachangia hivyo kuufanya Mfuko huu kujulikana pia kwa jina la Tele kwa Tele.  

Mfuko huu ulianza kwa majaribio wilayani Igunga mwaka 1996 na baadaye kuenea katika Halmashauri mbalimbali nchini ijapokuwa kasi yake imekuwa sio ya kuridhisha. Mwaka 2007 Serikali iliamua kuwa Shughuli za Mfuko huu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ziwianishwe.  

Hatua hii ilisababisha Serikali kuu mwezi Juni 2009 kukasimu mamlaka yake kitaifa ya kusimamia na kuendesha CHF  kuwa chini ya NHIF wakati Halmashauri zikiendelea na majukumu yake ya awali. 

Unaweza kusema kimsingi hasa nini maana ya maamuzi hayo na athari zake kwa wananchi?
Uamuzi huu unalengo la kuwezesha kutekeleza kwa kasi Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM 2007-2017), kuongeza uwigo na kuenea kwa CHF katika Halmashauri mbalimbali na pia kuboresha huduma ngazi ya Zahanati na Vituo vya Afya kwa sababu huduma zinazotolewa katika ngazi hizo zinawanufaisha wanachama wa Mifuko yote miwili.

Nataka kusema kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambao ndio wasimamizi wakuu wa CHF kitaifa, kiutaalamu na kiutawala waliona ni vyema kutumia uzoefu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, NHIF, na baraza la mawaziri liliagiza kukasimishwa madaraka ya kuratibu mifuko hiyo NHIF kwa lengo la kuoanisha shughuli zao, kuboresha huduma na kuongeza uwigo wa wananchi wanaohudumiwa na CHF hasa vijijini.

Je ni sheria iliyobadilishwa ama ni agizo na nini matokeo yake?
Si swala la mabadiliko ya kisheria ni utaratibu tu wa maagizo. Ukweli ni kuwa baada ya Wizara za WAUJ na  TAMISEMI kusaini hati ya maridhiano, Mfuko nao ulisaini tarehe 4/6/2009 na utekelezaji wake ulianza mwezi Julai, 2009. Mkataba huu wa usimamizi ni wa miaka 3 hadi tarehe 30 Juni, 2012.

Ili kutekeleza vyema jukumu hili Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umetayarisha Mpango kazi wa miaka 3 wa utekelezaji wa miaka mitatu kuanzia Julai 2009 hadi Juni 2012.

Pamoja na maelezo hayo mtu akikuuliza nini hasa maana ya Mfuko wa Afya ya Jamii na umelenga kusaidia nini hapa nchini unaweza kufafanua vipi?
Ni rahisi ni kama nilivyosema hapo awali  lakini kwa ufupi Mfuko wa Afya ya Jamii ni mfuko ambao unatoa huduma za matibabu kwa jamii ambayo haipo katika sekta isiyo rasmi wilayani, Tarafani na katika Kata na kijijini. Huu ni Mpango wa hiari ya uchangiaji wa huduma za matibabu ya kaya/familia kabla ya kuugua.

Mtu akiojiunga katika mfuko huu na kuitoa fedha ataihudumiwa yeye na Kaya yake au familia kwa mwaka mzima bila ya nyongeza ya malipo ya ziada kwa huduma zilizopo katika eneo husika.

Nini chimbuko la mifuko hii hapa nchini?
Chimbuko lake bwana mwandishi ni sawa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambalo ni kupungua kwa rasilimali na vyanzo vya mapato vya kuhudumia sekta ya afya hivyo kusababisha kudorora kwa huduma hiyo kwa wananchi.

Hili ni rahisi sana kulielewa.Katika  utafiti uliofanywa mwaka 1995 ulionyesha kuwa gharama za matibabu kwa kaya zilikuwa shilingi 17,000.00 kwa mwaka wakati uwezo wa Kaya kulipia matibabu hayo ilikuwa ni shilingi 5,000.oo na wakati huo huo Serikali ilikuwa inagharamia huduma za matibabu kwa Kaya kwa kiasi cha Shilingi 7,000.00 kwa mfumo ambao umekuwa maarufu kama Tele kwa tele.

Kihistoria Mfuko wa Jamii  hii CHF tunayoizungumza ilianzia kwa majaribio Wilayani Igunga mwaka 1996 na baada ya miaka miwili ukasambazwa katika halmashauri 9 na mwaka 2001 Bunge likapitisha muswada ulioanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii baada ya kuonekana kwamba ndio jibu la matatizo ya kupungua kwa uwezo wa serikali kuhudumia wananchi wake.

ila kinachoanzishwa kimsingi huwa na madhumuni yake.Ukiangalia dhumuni lenu ni kutoa tiba,lakini kwa mgonjwa tiba ni zaidi ya huduma anayostahili kupewa je waweza kufafanua hicho?
Ni sawa kabisa dhumuni letu ni kutoa tiba na hii tunaifanya kwa kuwezesha Kupungua pengo la fedha za matumizi katika huduma za afya zinazohudumiwa na Serikali kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe kwa huduma zinazowahusu katika uchangiaji nafuu na rahisi  na katika usimamizi wake. Pia dhumuni jingine ni kuboresha huduma za afya  kwa kuwezesha kupatikana kwa Watumishi, Dawa, Vifaa, Majengo  na kwa mantiki hiyo kuwezesha kuwapo kwa jamii  yenye afya na kupunguza vifo.

Ni vyema tukatambua kwamba mpango mzima umelenga kutoa madaraka kwa jamii katika katika ushirikishwaji wa mipango na maamuzi muhimu.Ni ukweli usipingika kwamba mpango huu ulibuniwa kwa lengo la kuwaepusha wananchi walio wengi vijijini na utaratibu wa kuchangia malipo ya papo kwa papo ambayo huwa yanaambatana na adha ya kuugua au kuwa na mgojwa na wakati huo huo unalazimika kutafuta fedha za kuchangia.

Kila kitu kina dhana na misingi mikuu. Je nini dhana na misingi ya Mifuko ya Jamii?
Inafaa kutambua tangu awali kwamba dhana na misingi ya Mifuko ya jamii  ni hiari na uwajibikaji. Mifuko hii inafanya kazi katika misingi ya ushirikiano na mshikamano ya Bima ya Afya ya Jamii.

Aidha Kadi hutolewa kwa Kaya ikijumuisha Baba, Mama na watoto chini ya miaka 18 na katika hili mtu wa kuanzia miaka 18 anahesabika kama kaya.Pia kiwango cha michango chini ya CHF kinaamuliwa na wananchi kupitia Bodi ya Afya ya Halmashauri na serikali ina serikali inatoa mchango wa tele kwa tele kulingana na fedha inayochangiwa.Halmashauri inapaswa kulipia gharama za matibabu za wote waliosamehewa kwa mujibu wa Misingi ya Kisheria na hati za makubaliano.

Kuna kitu kinaitwa Tika je unaweza kukielezaje?
TIKA ambayo ni huduma za matibabu katika miji na manispaa (TIKA-Tiba kwa Kadi) ni utaratibu ambao umeanzishwa lakini haujashika kasi.Utaratibu huu bado katika miji mingi kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhamasishaji mdogo na mazingira ya miji yalivyo tofauti na vijijini.

Waweza kuniambia Uwiano na tofauti iliyopo kati ya mfuko wa NHIF na CHF?
Mifuko yote miwili iko chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii;NHIF/CHF yote inasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya;Inafanya kazi kwa Pamoja na kusaidiana ngazi ya nchini katika kuboresha huduma. Mahali ambapo CHF inafanya vizuri, NHIF pia inafanya vizuri.

Unaweza kunieleza manufaa ya mifuko ya Afya ya jamii?
Kitu cha kwanza ni kutambua ukweli kuwa wananchi katika hili wanamilikishwa uendeshaji wa Mfuko na huduma za afya kwa ujumla, hali ambayo inaweza kabisa kujua na kutatua tatizo la ukosefu wa dawa muhimu.Hali hiyo ya kuwa mwanachama inamsaidia mwananchi kwa kiasi kikubwa kuwa na uhakika wa matibabu japo hana fedha baada ya kutoa mchango wake mara moja.

Kuwapo kwa mamlaka hayo kunasaidia ukarabati wa vituo vya afya vya kutolea huduma za afya kufanyika na kusaidia ulinzi wa vituo vya huduma ya Afya na kwa kweli kama CHF ikitekelezwa vizuri inaweza kuwa Mkombozi wa kweli afya ya Jamii kuelekea Afya bora kwa wote.

Unaweza kuniambia hali ya utekelezaji wa mifuko hiyo kwa sasa?
Hali ya utekelezaji wa Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF) hadi kufikia mwezi April, 2010 imeonyesha kuwa kwa sasa CHF inahudumia takribani Watanzania milioni 1.3. Siwezi kujivuna sana kwa hili  kutokana na ukweli kuwa takwimu hizi zinahitaji kuthibitishwa zaidi kwa vielelezo.

Lakini labda nikueleze kitu kimoja. Ili kujenga mfumo imara kwa ajili ya huduma bora, tumepanga kuwa na miradi ambayo itatekelezwa na NHIF kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.Miradi hii ni pamoja na kuweka muundo imara wa usimamizi wa CHF , Ushirikishwaji zaidi ,kufanikisha huduma zipatikane kwa urahisi na ziboreshwe hasa dawa na huduma za vipimo hususan vijijini.

Ingawa changamoto bado zipo nyingi unaweza kuytataja angalau kw aufupi mafanikio yaliyopatikana hadi sasa?
Yapo mafanikio pamoja na muda mdogo wa uhai wake. Lakini baadhi ya mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa ni pamoja na kubaini changamoto halisi zinazoukabili Mfuko wa CHF,Kuwa na mpango wa utekelezaji wa miaka 3 unaoendelea kutekelezwa na Kuanza kujenga uwezo wa watumishi wa ndani wa Mfuko wa Kanda na makao makuu kuhudumia wananchi

Pia tumefanikiwa kujenga uwezo wa ndani wa watumishi na maafisa waandamizi wa Mfuko na Kanda kuweza kufahamu kwa undani utekelezaji wa CHF na kuanza utekelezaji wake mara moja na kwa kujiamini na kuhamasisha Halmashauri zilizosalia zinatekeleza mpango wa CHF na baadaye kuzishitua Bodi zinazosinzia

Mnaimarishaje CHF kupitia usimamizi na uratibu wa NHIF?
Uimarisha wa huduma za Mifuko ya CHF, unafanyika katika maeneo mbalimbali. Hatua za awali za uimarishaji ambazo zimechukuliwa mpaka sasa ni kuhakikisha utaratibu wa Mifuko ya afya ya Jamii (CHF) unaenea katika Halmashauri zote ili wakulima wote nchini waweze kujiunga na huduma hii.

Mpango wa utekelezaji wa Mifuko ya CHF unaendelea kuuzwa na kujadiliwa na wadau wote muhimu ili kila mmoja ashiriki na awajibike katika maeneo yatakayomuhusu kwa pamoja kwa kuhakikisha Programu ya Elimu ya Kata-Kwa-Kata sasa inajumuisha elimu ya CHF na kuhakikisha wakulima wengi wanajiunga na CHF.

Ili kufanikisha zaidi na kuleta imani Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) katika mwaka 2009/2010 umetenga kiasi cha bilioni 3 kwa ajili ya mikopo nafuu ya vifaa tiba. Kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kinaweza kutumika kwa ajili ya kuvikopesha vituo vya matibabu vya msingi (zahanati na vituo vya afya- vijijini). Uhamasishaji kwa viongozi wa ngazi ya Halmashauri ili watumie fursa hii unaendelea. Huduma za vipimo ni za muhimu ili kuwapa wakulima tiba sahihi katika maeneo yao.