Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umebaini uwepo wa taarifa za upotoshwaji kupitia mtandao wa Jamii Forum, taarifa ambayo imeendelea pia kusambazwa kupitia mitandao mingine ya kijamii. Taarifa hiyo inadai kwamba NHIF hoi, watunga muswada kuinusuru, mashirika makubwa kama TANESCO, BoT, TRA, TPA kujiunga kwa lazima”. Tunapenda kuutarifu Umma kuwa taarifa hiyo si ya ukweli na imejaa upotoshaji kwa Umma. Mfuko unapenda kutoa ufafanuzi wa hoja zilizopo katika taarifa hiyo kama ifuatavyo:-

  1. Ucheleweshaji wa ulipaji wa Madai kwa kukosa fedha na kupelekea wanachama kunyimwa huduma za matibabu;

Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko huu, malipo kwa Watoa huduma waliosajiliwa na Mfuko yanatakiwa kulipwa ndani ya siku 60 tangu kuwasilishwa kwake. Lengo ni kutoa muda kwa Mfuko kuhakiki uhalali wa madai yanayowasilishwa na watoa huduma kabla ya kuyalipa. Hata hivyo, Mfuko umeendelea kuboresha mifumo yake ya TEHAMA ya ulipaji madai inayowezesha ulipaji wa madai ndani ya kipindi husika. Hivyo si kweli kwamba Mfuko hauna fedha za kulipa madai, bali madai hulipwa pale ambapo taratibu za kuhakiki zinapokuwa zimekalimilika.

Kuhusu wanachama kunyimwa huduma, Mfuko una mikataba na watoa huduma inayowataka kutoa huduma bora kwa wanachama wake. Endapo mtoa huduma anakwenda kinyume na makubaliano hayo, Mfuko huchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kusitisha mkataba kwa kituo husika. Hivyo, wanachama wanashauriwa kutoa taarifa pindi wanaponyimwa au kupata huduma zisizoridhisha, ili hatua stahiki zichukuliwe.

  1. Wigo mdogo wa huduma zitolewezo kwa wanachama;

Mfuko umeendelea kufanya maboresho katika kitita cha mafao yatolewayo kwa wanufaika kwa kuzingatia maoni ya wadau wake wakiwemo wanachama, watoa huduma, waajiri n.k. Kwa sasa Mfuko unatoa wigo mpana wa huduma za matibabu, katika vituo zaidi ya 6998, zikiwemo huduma za vipimo vikubwa kama vile MRI, CT-Scan, huduma za kusafisha figo (Dialysis), Upasuaji mkubwa wa kitaalamu ikwemo moyo, mishipa ya fahamu na uzazi, Matibabu ya Saratani na gharama za kumuona daktari wakiwemo madaktari bingwa. Aidha, Mfuko unatoa bima ya afya kwa wanachama wastaafu na wenza wao hadi mwisho wa maisha yao pasipo kuendelea kuchangia, utaratibu ambao hautolewi na Bima zilizo nyingi;

  1. Kuwasilisha muswada Bungeni ili kulazimisha mashirika makubwa ya Umma kujiunga na NHIF;

Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, inaelekeza watumishi wote wa Umma, walio katika Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika ya Umma n.k. kutakiwa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuchangia asilimia 3 ya mshahara na mwajiri kuchangia asilimia 3. Hivyo katika kutekeleza matakwa ya Sheria, Mfuko unaendelea na utoaji wa elimu kwa makundi haya ili nao waweze kuhudumiwa na Mfuko kulingana na sheria. Kupitia utaratibu huu, Taasisi na Mashirika ya Umma yenye Hospitali zake husajiliwa na Mfuko ili kuendelea kuwahudumia watumishi wake kupitia utaratibu wa bima ya afya.

Kuhusu uwasilishaji wa muswada Bungeni, Baada ya wananchi walio katika Sekta iliyo rasmi kupata huduma chini ya Mfuko, Serikali inatafuta namna bora ya kuwahudumia pia wananchi walio katika Sekta isiyo rasmi. Ni katika muktadha huo, Serikali inalenga kutekeleza MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE, ambao kwa sasa uko katika hatua za majadiliano ndani ya Serikali.

Mfuko unapenda kuwahakikishia wanachama wake na Umma wa Watanzania kwa ujumla kuwa, upo imara na kulingana na tathmini za uhai wa Mfuko (Actuarial Valuation), huduma za mfuko bado ni endelevu na unao uwezo wa kuwahudumia wanachama pamoja na wanachama wake wastaafu hadi mwisho wa maisha yao. Kwa hiyo, suala la Mfuko kuwa hoi na kushindwa kuwalipa watoa huduma wake si ukweli kama ilivyoandikwa katika mitandao ya kijamii. Kwa maelezo zaidi wanachama na wananchi kwa ujumla wanaweza kutembelea Ofisi za NHIF zilizopo karibu nao au kwa kupiga simu bure kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 0800 110063, barua pepe This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. au kwa kutembelea tovuti yetu www.nhif.or.tz.

 

Bernard H. Konga

KAIMU MKURUGENZI MKUU

29 Machi 2017