WACHEZAJI wa Timu ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ wamejiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo kuanzia sasa wana fursa ya kutumia huduma za matibabu popote walipo ndani ya nchi.

Jumla ya wachezaji 23 walikabidhiwa kadi hizo jana Makao Makuu ya Mfuko na Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Anjela Mziray ambaye alisema kuwa kitendo hicho ni fursa kwao kutumia huduma na kutangaza shughuli za Mfuko.

Mziray alisema kuwa kwa kipindi kirefu Mfuko umekuwa ukishirikiana kwa karibu na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kutokana na ukweli kwamba Michezo ni moja ya nguzo kubwa katika afya. Mbali na hilo pia alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa timu hiyo ambayo kwa sasa inaleta heshima kubwa ndani ya yetu. 

Akizungumzia umuhimu wa kuwa na kadi ya matibabu ya NHIF, alisema kuwa ugonjwa huja bila taarifa yoyote hivyo kitendo cha kuwa na kadi ya matibabu kinamwezesha mtu mwenye nayo kupata matibabu bila usumbufu wa aina yoyote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesiga alisema kuwa Kadi hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa wachezaji hao kutokana na ukweli kwamba wataweza kupata matibabu mahali popote nchini hata wasipokuwa kambini. 

“Tunaushukuru sana Mfuko kwa kuanzisha mpango huu ambao umewawezesha hata hawa vijana wetu kupata kadi za matibabu hivyo tunaendeleza huu ushirikiano kwa lengo pia la kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko,” alisema Mwesiga.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) Selestine Mwesiga akizungumza kwenye hafla ya kukabidhiwa kadi za matibabu kwa Timu ya Vijana ‘Serengeti Boys’

 

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Anjela Mziray akikabidhi kadi ya matibabu kwa vijana hao.

Viongozi wa TFF, NHIF na vijana wa Serengeti Boys mara baada ya kukabidhiwa kadi za matibabu.